Moi University Journals
Not a member yet
344 research outputs found
Sort by
Changamoto za Mbinu za Kutathmini Tafsiri
Matokeo yoyote ya tafsiri ni vizuri yapimwe ufaafu wake kabla ya kupelekwa kwa watumiaji. Hii ni kwa ajili ya kujiridhisha kama kazi aliyoifanya mfasiri ina ubora unaotarajiwa kwa matumizi ya walengwa. Katika makala haya tumeangazia changamoto za matumizi ya mbinu nne za kutathmini tafsiri ambazo ni kufanya tafsiri rejeshi, kupima uelewekaji, kupima uasili na kupima ulinganifu. Mbinu hizi zimebainika kuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ugumu wa utekelezekaji wa madai ya mbinu husika na kubana matumizi ya lugha. Msimamo wa makala haya ni kwamba, uamuzi wa mbinu ipi itumike kutathmini matini fulani ya tafsiri unapaswa kuongozwa na mbinu na nadharia iliyotumika kutafsiri matini husika. Hii ni kwa sababu mbinu na nadharia iliyotumika kutafsiri matini fulani ina athari kubwa katika matokeo, mwonekano na ujumbe wa matini lengwa. Aidha, katika makala haya inasisitizwa kwamba ni muhimu zaidi kwa yeyote anayetathmini matini ya tafsiri kutumia mbinu zaidi ya moja kutathmini matini moja ili kupata matokeo bora na yenye uhalisia. Vilevile, tumependekeza mbinu nyingine ya kutathmini tafsiri ambayo tumeiita mbinu ya uakifishaji
Mchango wa Mbinu ya Familia Wenyeji katika Ufundishaji na Ujifunzaji Darasani wa Kiswahili kama Lugha ya Kigeni
Familia Wenyeji ni moja kati ya mbinu mashuhuri zinazotumika katika ufundishaji wa lugha za kigeni kwa kuzingatia ufundishaji kimawasiliano. Tafiti mbalimbali zimeonesha umuhimu na ufaafu wa mbinu hii katika maendeleo ya ujifunzaji lugha kwa wajifunzaji wa lugha ya kigeni. Licha ya kuwepo uhusiano kati ya mbinu hii na ufundishaji na ujifunzaji wa lugha darasani, tafiti hizo hazikuonesha mchango wa matumizi ya mbinu hiyo katika ufundishaji na ujifunzaji wa lugha ya kigeni darasani. Makala hii imebainisha mchango wa mbinu hiyo katika ufundishaji na ujifunzaji wa darasani wa Kiswahili kama lugha ya kigeni kwa kuchunguza ni kwa namna gani walimu na wajifunzaji wanatumia familia wenyeji kama mbinu ya kufanikisha mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji wa darasani. Data za makala hii zimetokana na mahojiano yaliyofanyika kwa kuhusisha walimu wa Kiswahili kwa wageni, wajifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni na waratibu wa familia wenyeji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar na Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (MS TCDC) na kuchambuliwa kwa mkabala wa kimaelezo na kuongozwa na Nadharia ya Umahiri wa Kimawasiliano na Tamaduni Mchanganyiko ya Hall (1992). Matokeo ya utafiti yaliyojadiliwa katika makala hii yameonesha upo mchango wa matumizi ya mbinu hii katika ufundishaji na ujifunzaji wa Kiswahili kama lugha ya kigeni darasani
Siasa, Uchumi na Ustawi wa Jamii: Mtazamo wa Kisemiotiki wa Ushairi wa Kivumba
Makala hii inachunguza nafasi ya ushairi katika kuzungumzia masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni pamoja na ustawi wa jamii kupitia ushairi wa Kivumba. Ili kukuza mjadala wetu, makala hii ilifafanua ishara na maana katika ushairi wa Kivumba kwa kutumia nadharia ya semiotiki kutumia misimbo ya Barthes. Lengo la mjadala wetu ni kubainisha ya kwamba, ushairi unaweza kuwa chombo mbadala cha kuzungumzia masuala yanayoikumba jamii kikamilifu. Makala hii inazingatia kauli kwamba, malighafi makuu ya fasihi simulizi ni jamii. Makala hii inajadili kwamba, sio rahisi kufasiri ishara na maana katika ushairi wa jamii yoyote nje ya mkutadha wa jamii yenyewe. Ili kuongoza mjadala huu, mjadala ulijikita katika ushairi wa Kivumba pekee kwa kutumia misimbo mitano ya Barthes. Ushahidi wote uliotegemewa katika mjadala wetu ni ule uliotokana na mifano iliyokusanywa kutoka nyanjani katika maeneo ambapo Kivumba kinazungumzwa nchini Kenya baina ya 1919-2020
\u27Sipangwingwi, Watajua Hawajui\u27: Jaribio la Kuelekeza Matumizi ya Lugha Dhidi ya Uhalisia wa Kiisimujamii
Makala haya yanaangazia nyimbo mbili, ‘Sipangwingwi’ na ‘Watajua hawajui’ ambamo mnapatikana maneno mawili Sipangwingwi na Watajua hawajui. Hivi karibuni, Serikali ya Kenya, kupitia Shirika la NCIC imetoa tamko ambalo linaharamisha matumizi ya haya maneno mawili, miongoni mwa mengine kwa madai kwamba huenda yanaweza kuibua hisia fulani ambazo zinaweza kuchangia hali ya machafuko katika na baina ya Jamii-tumizi lugha mbalimbali. Makala haya basi yanajadili matumizi ya vifungu hivi viwili kwa kurejelea nyimbo hizo mbili ambapo waandishi wamejaribu kuonyesha kwamba ni makosa kuelekeza matumizi ya lugha, kwa kuwalazimisha wanajamii kutotumia maneno fulani ambayo, huenda yanatumiwa kwa wingi na mtu au mwanasiasa fulani. Ukweli wa kiisimujamii ni kwamba, lugha inafaa kujiendeleza, kujikuza na kujisambaza kote, kutegemea watumiaji wake, katika muktadha wowote: sokoni, kanisani, msikitini, mtaani, na kwingineko
Mchakato wa Uchopezi katika Utohozi wa Maneno ya Kireno Yaliyoingia katika Kiswahili
Kutokana na kutofautiana kwa lugha ya Kireno na Kiswahili, maneno ya Kireno yanapoingia katika Kiswahili hulazimika kutoholewa ili yafanane na muundo wa Kiswahili na yaweze kukubalika. Mchakato wa uchopezi ni mojawapo kati ya michakato maarufu inayotumika katika utohozi wa manenomkopo. Kwa msingi huo, makala hii imechambua kwa kina aina mbalimbali za uchopezi zilizotokea wakati wa utohozi wa maneno ya Kireno yaliyoingia katika Kiswahili. Data za makala hii zimekusanywa kwa kutumia majadiliano ya kikundi lengwa yaliyohusisha wanaetimolojia 3 na uchambuzi wa nyaraka uliohusisha kamusi ya Johnson (1939), makala ya Prata (1983) na kamusi ya TUKI (2019) zilizopatikana kwa njia ya kukusudia. Kwa kutumia NFUU, makala imebaini kutokea kwa uchopezi mwanzo, kati na paragoji wakati maneno ya Kireno yalipoingia katika Kiswahili. Kati ya aina hizo, uchopezi kati hasa ule wa anaptiksis kabla ya kimadende hutokea zaidi kuliko aina nyingine. Aidha, katika aina za sauti zinazochopekwa, uchopezi wa irabu hutumika zaidi ukilinganisha na uchopezi wa konsonanti na irabu ya juu nyuma viringe [u] ndiyo inayotumika zaidi wakati irabu ya kati nyuma viringe [ɔ] haitumiki sana. Kutokana na matokeo hayo, makala hii inapendekeza kuwa ukopaji ni njia muhimu ya kupanua msamiati wa lugha. Kwa hiyo, hauna budi kuchukuliwa kwa mtazamo chanya. Halikadhalika, NFUU ni vyema ikazingatiwa katika uchambuzi wa mabadiliko ya lugha kutokana na umuhimu wake wa kuyahalalisha maumbo ya lugha ngeni kukubalika katika lugha pokezi
Uchanganuzi wa Mkazo katika Maneno ya Kiswahili Sanifu
Makala haya yamechukuza udhihirikaji wa mkazo katika maneno ya Kiswahili Sanifu ili kuweza kubaini utokeaji wa mkazo katika neno. Lengo hasa ilikuwa kuchunguza namna mkazo unavyojibainisha katika neno. Utafiti huu ulilenga kuchunguza mkazo katika Kiswahili sanifu. Hii inatokana na namna mkazo unavyojitokeza kwa kuonesha msigano wa nguvumsikiko baina ya viambajengo vinavyohusika katika neno yaani silabi. Uchunguzi huu unashadidiwa na uchanganuzi wa mkazo kinadharia kuwa kila kiambajengo kina nguvumsikiko fulani ambayo husababisha kuwepo na aina za mkazo. Data zilikusanywa uwandani kwa njia ya mahojiano na ushuhudiaji. Mbinu zilizotumika katika uchanganuzi wa data ni mkabala wa kimaelezo na kiidadi. Nadharia ya Fonolojia Mizani (FM) imetumika katika uchanganuzi wa data. Data zimewasilishwa na kufanyiwa uchanganuzi kwa kutumia mifano, vielelezo, michoro na ufafanuzi. Matokeo yanaonesha kuwa mkazo uliokuwa unashughulikiwa katika tafiti zilizotangulia ni mkazo msingi tu, bila kuhusisha mkazo katika silabi nyingine ambazo zinapotamkwa huwa na nguvumsikiko fulani wakati wa utamkaji. Kwa mantiki hiyo silabi nyingine nazo zina mkazo. Hivyo, kuweza kuwa na mkazo upili, utatu na kadhalika kutegemea na viambajengo katika neno husika. Aidha, utokeaji wa mkazo katika viwango tofauti tofauti kati ya silabi zinazounda neno husika imetudhihirishia kuwa kiuchanganuzi katika Kiswahili sanifu kuna aina za mkazo kutegemeana na kiwango cha nguvumsikiko
To Translate or Not to Translate Interjections as Hedges: A Case Study of Kenya’s Political Speeches
This paper investigates the occurrence of interjections as hedges in Kenya\u27s presidential political speeches and their translatability from English into Kiswahili from a skopos based perspective. These hedges have a significant pragmatic functionality that cannot be ignored even in translation. The paper explores the usage of this kind of a hedge in the presidential political speeches in Kenya and what effect arises from its translatability or non-translatability. As a communicative feature that carries an indirect meaning, hedges play a significant role in message delivery, a functionality that makes them important in a discussion. As opined by Lakoff (1972), hedges’ functionality is beyond the fuzzy notion, carrying an important meaning that would have otherwise not possible to deliver it devoid of these hedges. Pragmatically, this linguistic feature has been referred to in different terms such as shields, indeterminants and expression of politeness (Halliday 1994, Levinson 2000). In this regard, their functionality is a necessary ingredient in communication process which cannot be ignored. This research has been carried out in reference to Skopo’s theory whose tenetes of purpose, optimality, faithfulness and cohesion looks at the usage of these words and their transferability from English to Kiswahili in Kenyan’s political speeches since their presence in a communication process generally is and often has been viewed as nuisance. Twenty speeches from Kenya’s presidential candidates in 2013 and 2017 together with their running mates were transcribed. The units of meaning with interjections were identified and subjected to translation from English into Kiswahili. It was found that translation strategies largely used ware literal translation, omission and domestication although other approaches were still available in rendition of the required meaning
Dhima ya Viambishi Ngeli za Nomino za Ki-Vunjo
Makala haya yanashughulikia dhima ya viambishi ngeli za nomino za ki-Vunjo. Utafiti kuhusu makala haya ulifanyika Kaskazini Mashariki mwa Tanzania mkoani Kilimanjaro katika wilaya ya Moshi Vijijini. Mbinu ya Usampulishaji Nasibu Pangilifu ilitumika katika utafiti huu katika kupanga umri na jinsi, ambapo jinsi ya kike wamehusika watoa taarifa 15 na jinsi ya kiume wamehusika watoa taarifa 15. Watoa taarifa wote 30 walikuwa wazungumzaji wa ki-Vunjo wenye umri kati ya miaka 44-74. Taarifa zimekusanywa kwa watoa taarifa kwa kutumia njia za hojaji, usaili na ushuhudiaji. Utafiti huu ulilenga kubainisha dhima ya viambishi ngeli za ki-Vunjo. Ili kutimiza lengo hili, Mkabala wa Kisemantiki ulitumika sambamba na Nadharia ya Mofolojia Asilia (NMA) iliyopendekezwa na Dressler (1985) na Wurzel (1987). Matokeo ya utafiti huu yamebaini kuwa lugha ya ki-Vunjo ina idadi ya ngeli 18 ambapo imebainika kuwa katika viambishi ngeli kuna dhima mbalimbali zinazojitokeza zaidi ya umoja na wingi. Dhima hizo ni: ukubwa, udogo, uzuri na ubaya. Mwisho, utafiti huu umetoa mapendekezo ya tafiti fuatishi
Tathmini ya Programu ya \u27Tafsiri ya Google\u27 kama Zana ya Mfasiri: Changamoto na Mapendekezo
Mfasiri ni daraja muhimu linalounganisha utamaduni wa lugha ya matini chanzi na matini lengwa, hadhira chanzi na hadhira lengwa na pia jamii chanzi na jamii lengwa. Mchakato wa tafsiri huhusisha zana ambazo hutumiwa na mfasiri kama chanzo cha visawe vya lugha chanzi katika lugha lengwa. Moja wapo ya zana iliyozoeleka sana ni kamusi za lugha. Hata hivyo, kutokana na wimbi la utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kumejitokeza ubunifu na ugunduzi wa mifumo na nadharia mpya katika nyuga mbalimbali. Tafsiri kama taaluma haikuepuka kupokea ubunifu na ugunduzi huo. Hivyo, tumeshuhudia kuibuka kwa program tumizi mbalimbali za mifumo ya kielektroniki na teknolojia zinazotumika kama zana mpya za tafsiri. Miongoni mwa programu hizo ni Tafsiri ya Google, hii ni programu tumizi maarufu ya tafsiri inayotumiwa na wafasiri kama zana ya kutafsiri matini za lugha mbalimbali duniani. Kwa hiyo, makala hii inatathmini matumizi ya programu ya Tafsiri ya Google kama zana ya mfasiri kwa kuchunguza changamoto na kutoa mapendekezo. Makala inalenga kubainisha mdafao wa matumizi ya Tafsiri ya Google kama zana ya mfasiri, changamoto za programu ya Tafsiri ya Google katika tafsiri na kupendekeza suluhisho la kukabiliana na changamoto na matatizo ya kutumia programu za mifumo ya kielektroniki katika kutafsiri. Data za makala hii zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya upitiaji nyaraka na usaili. Aidha, uwasilishaji na uchambuzi wa data za makala hii umejiegemeza katika nadharia ya ulinganifu wa matini. Kwa ujumla makala hii inajadili kuwa program ya Tafsiri ya Google kama zana ya mfasiri ina changamoto zinazoifanya ikose sifa ya kuwa zana mbadala wa kamusi za lugha. Uchunguzi huu umebaini kuwa changamoto hizi zimejikita katika kisemantiki, kimofolojia, kisintaksia na mtindo wa lugha. Aidha, mfasiri anapotumia Programu ya Tafsiri ya Google kama zana ya tafsiri, anatakiwa kuzingatia misingi ya kinadharia na vitendo ili kuzalisha tafsiri bora na yenye ufanisi. Hivyo, ili kukidhi haja ya tafsiri, mfasiri anatakiwa awe na ujuzi na maarifa ya lugha zote mbili, utamaduni, muktadha, hadhira, malengo na mazingira ya tafsiri
Ujitokezaji wa Uradidi katika Lugha ya Kihaya: Uchunguzi wa Kategoria ya Vitenzi, Vielezi na Vivumishi
Makala haya yanachunguza uradidi unavyojitokeza katika lugha ya Kihaya kwa kuangazia kategoria ya vitenzi, vielezi na vivumishi. Mtafiti amekusanya data ya makala haya katika Mkoa wa Kagera, Wilaya ya Muleba Kata ya Izigo. Ameteua kata hii kwani ndiko inakozungamzwa Lahaja ya Kihamba inayoshughulikiwa na mtafiti wa makala haya. Halikadhalika, Kihaya kinatumiwa katika mawasiliano ya kawaida na shughuli nyingine nyingi za kiuchumi, kijamii nakadhalika. Mtafiti amekusanya data kwa kutumia mbinu za hojaji na uchambuzi wa matini. Mbinu ya kuchambua matini iliyotumika ni ile ya usomaji wa nyaraka za kitaaluma zilizompa mtafiti wigo wa kupata data faafu. Nyaraka zilizosomwa ni kama vile: tasnifu na maandiko mbalimbali. Hojaji hurejelea orodha ya maswali na maelekezo aliyoandaa mtafiti ambayo hujibiwa na watafitiwa, kwa lengo la kukusanya data faafu ya utafiti. Data ilichanganuliwa kwa kutumia mikabala ya maelezo na ufafanuzi. Aidha, makala haya yameongozwa na Nadharia ya Uelekeani iliyoasisiwa na McCarthy na Prince (1993, 1994a, 1994b na 1995). Matokeo ya makala haya yanaonesha kuwa uradidi hujitokeza katika kategoria za vitenzi, vielezi na vivumishi katika lugha ya Kihaya. Uradidi huo huweza kuhusisha neno zima au sehemu tu ya neno. Kwa vile makala haya yamechunguza sehemu tu ya uradidi katika lugha ya Kihaya, inapendekezwa utafiti ufanyike kuhusiana na kategoria nyinginezo kama vile nomino, vihusishi, vihisishi, viwakilishi nakadhalika