Moi University Journals
Not a member yet
    344 research outputs found

    Mikabala ya Uchanganuzi wa Hiponimia na Uainishaji Wake

    No full text
    Wataalamu mbalimbali wa Kiswahili wameshughulikia tafiti za hiponimia ya kategoria za nomino na vitenzi huku wakitoa mifano anuwai. Hata hivyo, tafiti hizo hazijadhihirisha mikabala inayoweza kutumiwa kuichanganua kama vile mkabala wa kisayansi na kiisimu. Vilevile hakuna mitindo ya uainishaji wa hiponimia ambayo imewahi kuangaziwa katika Kiswahili mbali na kutajataja tu hipanimu husika na zile hiponimu zake. Hivyo basi, makala hii imeshughulikia mikabala ya uchanganuzi wa hiponimia na uainishaji wake kwa kulenga leksimu za Kiswahili hasa za kategoria za nomino na vitenzi zilizoteuliwa kidhamirifu kutoka kamusi anuwai za Kiswahili. Makala hii imedhihirisha kuwa hiponimia inaweza kuchanganuliwa kwa kuzingatia mikabala miwili: mkabala wa kisayansi na kiisimu. Aidha, uainishaji wa hiponimia za kategoria za nomino na vitenzi huweza kufanywa kwa kuzingatia mkabala wa kiisimu katika misingi sita maalum kama vile: kitambuzi, kiuamilifu, kijiografia, kitukio, kihali na kitendo

    Mielekeo ya Lugha na Ruwaza za Matumizi ya Lugha ya Walimu wa Kiswahili wa Shule za Msingi katika Kaunti ya Siaya

    No full text
    Makala haya yalichunguza  na kubainisha mielekeo ya walimu wa Kiswahili katika shule za msingi za kaunti ya Siaya. Aidha, ruwaza zao za matumizi ya lugha zilipambanuliwa. Data ilikusanywa kwa kutumia hojaji. Wasailiwa 34 waliteuliwa kutoka kaunti ndogo sita za kaunti ya Siaya. Data ilichanganuliwa kwa mkabala mseto kwa kutumia njia za kitakwimu na kimaelezo.  Matokeo ya utafiti yamewasilishwa kupitia njia za maelezo na majedwali. Matokeo ya utafiti yameonesha kwamba walimu walikuwa na mielekeo kubalifu kuhusu Kiswahili. Aidha, ruwaza za matumizi yao ya lugha zilidhihirisha kwamba matumizi ya Kiswahili yamezidi kupanuka katika mawanda mengi ya kijamii katika Kaunti ya Siaya

    Filamu ya Kiswahili: Fasihi Simulizi Iliyostawi

    No full text
    Makala haya yanaijadili sanaa ya filamu za Kiswahili kama fasihi simulizi iliyopevuka na kuchukua mkondo wa kiteknolojia kutokana na utegemezi wake wa nyenzo za kisasa katika utambaji. Hadhi ya kisanaa ya filamu imetazamwa kwa namna inayoonesha kujitokeza kwake kupitia umbo na wajihi wa kifasihi. Filamu imeonekana kuwa jukwaa huru linaloruhusu sanaa tofauti zinazosindikiza ujenzi wa maudhui ya kifasihi kujipenyeza kusaidia kuutengeneza ujumi wa kifasihi. Kustawi kwa fasihi simulizi kupitia umbo la filamu kumechunguzwa kwa namna inavyodhihirisho taswira zilizo ndani ya bongo la mtambaji: anayezitoa na kuziweka katika picha jongefu ili mtazamaji azione runingani na kumfanya ayaone maumbo ambayo alipaswa kuyafasiri kulingana na mwendelezo wa simulizi. Ukuaji wa filamu ya Kiswahili umejadiliwa sanjari na udondokaji wa usomaji wa riwaya, tamthiliya, pamoja na ushukaji wa jumla wa kusoma nchini Tanzania. Licha ya filamu kuonekana kupiga kasi katika kueneza Kiswahili, ukuzaji wake umeonekana kutia shaka. Hivyo, imeonekana ni vyema somo la uandishi wa filamu liingizae katika mtalaa wa fasihi ya Kiswahili ili kuwajenga waandishi wa miswada ya filamu pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa wanaKiswahili. Mwishoni, manju wa fasihi simulizi ya Kiswahili wameshauriwa kuchangamkia kukua kwa teknolojia kimawasiliano na kiuhifadhi wa sanaa, fasihi na utamaduni

    Usawiri wa Familia ya Kisasa katika Fasihi ya Watoto Nchini Kenya

    No full text
    Madhumuni ya makala haya ni kuhoji kwamba licha ya kuwepo kwa familia za aina mbalimbali na zilizo changamano nchini Kenya, watunzi wa hadithi za watoto wanaendelea kusawiri familia kiini ambazo kimsingi huwa na baba, mama na watoto, ilhali kihalisia wapo watoto wanaotokana na familia za mzazi mmoja, familia za malezi na wengine kutoka taasisi za malezi na hata familia ambapo walezi wa watoto ni babu na nyanya za watoto wanaolelewa. Kwa misingi hii kunaweza kutolewa hoja kwamba fasihi ya watoto ya kisasa nchini Kenya haiwasilishi upana, uchangamano na usasa wa kifamilia kwa sababu tathmini za hadithi nyingi za watoto zilizoko zinadhihirisha uhalisi wa usawiri wa familia wa aina moja na kwa hivyo kuibua fikra potovu kwamba watoto kama wahusika katika tungo mbalimbali za fasihi ya watoto wanatoka katika familia zinazowiana. Uhalisi huu wa chukulizi potovu za uwepo wa familia kiini katika hadithi za watoto unadhihirika katika vitabu viwili teule vya fasihi ya watoto - ‘Mwepesi wa Kusahau’ na ‘Likizo ya Mkosi.’ Usawiri wa familia katika vitabu hivi umekitwa katika uelewa banifu kwamba kimsingi, familia huendesha shughuli za kila siku kama familia kiini - yaani familia inayojumuisha baba, mama na watoto, familia isiyokuwa na mahusiano na familia pana. Makala haya yanapania kupendekeza kwamba utunzi wa hadithi za watoto unahitaji ujasiri wa kusawiri mifumo anuwai ya kifamilia inayojitokeza katika hadithi za watoto katika upana wake wa kiuchangamano ili kuwezesha kuakisika kwa mifumo na miundo yote ya kifamilia inayopatikana nchini Kenya. Hii itawezesha usomaji wa fasihi ya watoto shuleni kwenda hatua zaidi ya burudani na kutilia mkazo usomaji unaojenga ukuaji wa mitazamo chanya ya maisha miongoni mwa watoto wakiwa wangali wadogo kuhusiana na usawiri wa familia. Makuzi ya watoto na ufunzaji wa maadili ni mambo yawezekanayo sio katika misingi ya familia tu bali pia kupitia mafunzo ya fasihi ya watoto

    Uchanganuzi wa Toni katika Ushairi wa Kithaka wa Mberia

    No full text
    Suala la mtazamo na hisia ni muhimu katika uhakiki wa fasihi hususan ushairi. Uchanganuzi wa mashairi hauna budi kutambua kuwa mshairi hutumia maneno na miundo ya sentensi ili kuwasilisha mtazamo au mawazo fulani. Kwa hivyo, ili kufahamu mawazo yanayowasilishwa na mshairi, ni muhimu kuchunguza toni ya mashairi yake. Baadhi ya maswali yanayodokeza toni ya mshairi ni haya yafuatayo. Je, mshairi anasema jambo fulani kutokana na matazaomo gani? Je, ikiwa shairi hilo lingesomwa hadharani, sauti yake ingesikika vipi? Je, mshairi “anaongea” kwa hasira, ucheshi au uchungu? Je, anatumia maneno au msamiati unaoelekeza? Tungo nyingi za kishairi hutegemea mbinu ambazo huziwezesha kuwasilisha ujumbe wake kwa athari kubwa. Huu hasa ndio msingi wa kuzungumzia hisia katika shairi. Suala la hisia huweza kufungamanishwa kwa kiasi kikubwa na dhana ya toni. Sauti inayosikika katika utungo wa kishairi huwa na mchango mkubwa katika uwasilishaji wa maana katika mashairi. Matarajio ya msomaji au msikilizaji ni kuwa utungo unaohusu jambo la huzuni, ucheshi, kinaya au uchungu utakuwa na uteuzi wa maneno, msamiati na sentensi zinazoweza kuibua athari iliyokusudiwa na mwandishi au mzungumzaji. Katika makala haya,  tunachanganua kipengele cha toni kwa undani kama kinavyojitokeza katika baadhi ya mashairi ya Kithaka wa Mberia katika diwani zaMchezo wa Karata(1997), Bara Jingine (2001), Redio na Mwezi (2005), Msimu wa Tisa (2007) na Rangi ya Anga (2014). Tunachanganua namna toni za uchungu, furaha, huzuni, tashtiti na kinaya zinadhihirika na ufaafu wake katika ujumbe anaouwasilisha mshairi

    Usawiri wa Upembezaji wa Mwanamke katika Bunilizi za Clara Momanyi

    No full text
    Makala haya yanahusu usawiri wa upembezaji wa mwanamke katika bunilizi za Clara Momanyi. Upembezwaji wa mwanamke ni suala ambalo limekithiri katika jamii nyingi za Kiafrika. Utamaduni hasi na ubabedume ni mambo ambayo yamechangia pakubwa upembezwaji huu. Hata hivyo, kwa kiwango fulani mwanamke mwenyewe amechangia hali hii kwa kujidunisha mwenyewe au kwa kukosa sauti na ujasiri wa kusimama kidete na kujiamulia mustakabali wake. Suala hili limejitokeza katika bunilizi za Clara Momanyi. Katika makala haya, nilihakiki hadithi fupi zifuatazo: ‘Ngome ya Nafsi’ kwenye diwani ya Mayai Waziri wa Maradhi na Hadithi Nyingine (2004) na riwaya ya Tumaini (2006)

    Usawiri wa Mwanamke katika Nyimbo za Sifo za Wakamba

    No full text
    Makala haya yanachambua usawiri wa mwanamke katika baadhi ya nyimbo za sifo za Wakamba nchini Kenya. Ili kufafanua namna mwanamke alivyosawiriwa na wasanii wa nyimbo hizi za sifo za Wakamba, tutawarejalea wasanii wachache wa nyimbo za sifo za Wakamba. Makala hii inaegemea  nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika. Nadharia hii imetumika kuongoza uchunguzi wa jinsi mwanamke Mwafrika  alivyosawiriwa na watunzi hawa wa nyimbo za sifo za Wakamba ambao ni watunzi wa Kiafrika. Watunzi wenyewe ni Bosco Mulwa, Justus Myello, Dan Mutuku, Kijana Mumo na Wanginga. Wasanii hawa waliteuliwa kimakusudi kutoka jamii ya Wakamba

    Kufanana na Kutofautiana kwa Konsonanti katika Msamiati wa Kipemba na Kingazija

    No full text
    Makala haya yanahusu ulinganishaji wa mfumo wa saui za konsonati baina ya Kipemba na Kingazija kwa lengo la kubaini mfanano na tofauti zilizopo baina yake. Data za makala haya zilikusanywa uwandani katika mazingira chasili ya wazawa wa lugha kupitia mbinu za hojaji na mahojiano. Matokeo tuliyoyapata kutoka kwa watoataarifa yameonesha kuwapo kwa mfanano na tofauti za mfumo wa sauti za konsonanti katika Kipemba na Kingazija. Hata hivyo, pamoja na tofauti za hapa na pale, tunathubutu kusema kuwa, Kipemba na Kingazija ni lugha ambazo zinatokana na lugha-mame moja, kwani tofauti hizo ndogondogo zilizojitokeza, imebainika kuwa zimetokana na utengano wake wa muda mrefu pamoja na umbali wa kijiografia uliopo miongoni mwake

    Uchanganuzi wa Ishara za Kisemiotiki zinazotumiwa katika Matangazo ya Biashara ya Kampuni ya Safaricom

    No full text
    Maendeleo ya teknolojia yamebadilisha sura ya matangazo ya biashara hasa kupitia kwa vyombo vya habari. Makala haya yanaangazia jinsi matangazo hutumia lugha pamoja na ishara za kisemiotiki ili kuwashawishi watazamaji wanunue bidhaa zinazotangazwa na kampuni ya Safaricom. Ishara hizo ni picha, rangi mbalimbali, mazingira, wahusika na elementi nyinginezo. Uchanganuzi wa ishara za kisemiotiki katika makala haya unaongozwa na nadharia ya Kress na van Leuween ya Muundo wa Ishara za Uoni (1996). Aidha, makala yanabainisha kuwa Kampuni ya Safaricom hutumia ishara nyingi za kisemotiki zinazotumiwa sambamba na lugha ili kuwashawishi wateja kununua bidhaa zao. Ishara hizo huundwa kwa ufundi mkubwa na huwa na maana fiche inayoeleweka kulingana na muktadha wa tangazo

    Ujenzi wa Ujitambuzinafsi Hasi katika Bunilizi za Omar Babu

    No full text
    Ujenzi wa ujitambuzinafsi ni suala ambalo limeshughulikiwa katika fasihi ya Kiswahili kiutunzi au kiutafiti. Suala hili hujitokeza kupitia kwa jinsi watunzi wa kazi za sanaa wanavyowasawiri wahusika kwa minajili ya kukuza maudhui. Usawiri wa wahusika huathiriwa na itikadi za jamii lengwa zikiwemo utamaduni hasi unaotia nguvu mfumo wa ki-ubabedume ambao umechangia pakubwa ujenzi wa ujitambuzinafsi huu. Hata hivyo, kwa kiwango fulani mwanamke mwenyewe amechangia hali hii kwa kujidunisha mwenyewe au kwa kukosa sauti na ujasiri wa kusimama kidete na kujiamulia mustakabali wake. Suala hili limejitokeza katika bunilizi za Omar Babu ambazo ni Kala Tufaha (2007), hadithi fupi ya ‘Ndoa ya Samani’ katika Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine (2010) na Heri Subira (2010). Katika bunilizi teule, mwandishi ameliangazia suala la ujenzi wa ujitambuzinafsi hasi wa jinsia ya kike kwa kiwango kikubwa. Ingawa mwandishi huyu anapania kujenga sauti ya mwanamke katika jamii iliyombana na mila zilizopitwa na wakati, katika makala hii tumelengakuonyesha na kutathmini namna ambavyo Babu amewasawiri wahusika wake ili kubainisha hali halisi ya mwanamke katika jamii husika. Uchanganuzi wetu umeongozwa na Ufeministi wa Kiafrika ambao ni mojawapo wa matapo ya Nadharia ya Ufeministi. Utamaduni unampa mwanamke nafasi gani katika jamii? Ni ipi taswira ya uhusiano wa mwanaume na mwanamke katika jamii ya Kiafrika? Je, mwanamke amechangia kwa njia gani hali yake? Tunapania kuyajibu maswali haya katika Makala haya

    145

    full texts

    344

    metadata records
    Updated in last 30 days.
    Moi University Journals
    Access Repository Dashboard
    Do you manage Open Research Online? Become a CORE Member to access insider analytics, issue reports and manage access to outputs from your repository in the CORE Repository Dashboard! 👇